Siasa za udini zabisha hodi Kilimanjaro

Mgombea wa CCM aliyeongoza kura za maoni Jimbo la Moshi Mjini, Ibrahim Shayo amekutana kwa siri na masheikh watatu wa BAKWATA akisaka kupata ushawishi wao ili aweze kupitishwa na vikao vya juu vya chama hicho.

Katika kikao chao cha siri kilichofanyika  Julai 29, 2020 taarifa zetu zinabainisha kuwa wamekubaliana kwamba kila linalowezekana lifanyike ili jina la mgombea huyo lirejeshwe na hatimaye kuwa mgombea ubunge.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa mgombea huyo amejawa hofu kutokana na kucheza rafu kwa miaka minne akifanya kampeni na kugawa rushwa kwa wajumbe huku akilindwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Patrick Boisafi.

Shayo amewaomba masheikh kumwendea Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya kichama ya Moshi Mjini, Alhaji Omary Shamba awashawishi BAKWATA Mkoa, waibebe agenda hiyo hadi kwa Mufti wa Tanzania.

Katika mkutano wao, pia wamekubaliana kuwa Mufti Sheikh Abubakar Zuberi naye abebe ajenda hiyo hadi kwa Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Magufuli ili asaidie jina kurudi.

Mmoja wa masheikh aliyeshiriki kikao hicho hakupendezwa na kinachoombwa kifanyike na alitoa taarifa kwa vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa kuwa ni hatari kupitisha mgombea kwa udini.

Juzi hiyohiyo, mgombea huyo amesikika akisema mwaka 2014 hadi 2017 yeye na mfanyabiashara anayemiliki kampuni ya Dema Construction walimlipia mkopo Mwenyekiti wa CCM mkoa, Patrick Boisafi.

Boisafi inadaiwa alichukua mkopo wa kibiashara benki ya CRDB kwa ajili ya kujenga eneo la kibiashara la Kili Home, lakini sehemu kubwa ya fedha hizo akazipeleka kijijini kwake Kibosho na kujenga nyumba ya ghorofa.

Imeelezwa kuwa alishindwa kulipa mkopo huo na yeye na Dema Construction wakamsaidia, basi Boisafi kwa vyovyote vile hatakubali vikao vya kamati za siasa vikate jina lake, kama fadhila ya kumsaidia.

Mgombea huyo ambaye ameapa kuutaka kwa udi na uvumba ubunge wa Moshi mjini kwa gharama yoyote, anatamba pia kwamba yeye ndiye aliyemwingiza madarakani Boisafi hivyo ni kipindi cha kulipa fadhila.

Japokuwa anafanya kila linalowezekana jina lake lisikatwe na pia awekewe alama nzuri vikao vya kamati ya siasa.

Jimbo la Mwanga nako fukuto

Katibu wa CCM wa Wilaya ya Mwanga, Sixtus Mosha anatuhumiwa kuchukua mlungula ili kupindisha taratibu za uchaguzi Kata ya Shighatini ili kumbeba Salehe Riziki Mkwizu.

Mkwizu ndiye aliyeshinda na mmoja wa wagombea walioshiriki kura za maoni jimbo la Mwanga.

Inaelezwa kuwa Shabibu Mruma amepanga kumfanya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mwanga.

Ingawa sheria inataka diwani wa Kata awe mkazi ndani ya Halmashauri husika, lakini Salehe Riziki Mkwizu anaishi Arusha na Katibu alifanya kampeni akitaka wajumbe wachague mtu mwenye uwezo wa kifedha.

Wakati wa kujinadi, Riziki Mkwizu alikiuka waziwazi kanuni kwa kutumia bango lenye nembo na rangi ya CCM wakati wagombea wengine wote walipewa karatasi nyeupe zilizoandikwa kwa mkono.

Hii inadaiwa ilimfanya aonekane tofauti na wagombea wengine wote na kujenga taswira kuwa ndiye anayetakiwa na CCM.

Yote haya yamefanyika chini ya ufadhili wa Shabibu Mruma ambaye anatuhumiwa kuwa na digrii aliyoipata baada ya kugushi taaluma yake hali iliyosababisha chuo kikuu cha Mzumbe kumfutia digrii hiyo.