Magufuli, Museveni wakubaliana kuufufua mradi wa Bomba la Mafuta

Rais John Magufuli na mwenzake wa Uganda, Yoweri Museveni wamekubaliana kurejesha kwenye Ikulu zao mchakato wa kutandaza bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki.

Bomba hilo linaloanzia Hoima, Uganda na kuishia Chongoleani, Tanga nchini Tanzania, limekwama baada ya kuwepo kwa “vizingiti” ndani ya serikali zao na  hata wawekezaji katika mradi huo.

Wawekezaji katika mradi huo mkubwa wa kusafirisha mafuta, ni Total, Tullow na Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya China.

Kukwama kwa mradi huo uliopangwa kukamilika mwishoni mwa mwaka jana, kumechangiwa na kile kinachoelezwa ni “mgogoro wa kodi” kati ya Uganda na mwekezaji Tullow, hasa juu ya kodi ya mapato baada ya kuuza hisa zake kwa Total. Hata hivyo, mgogoro huu umemalizwa baada ya Tullow kuuza hisa zake kwa Total, ambayo inaridhia kulipa kodi hiyo kwa Uganda.

Aidha, inaelezwa kuwa kusuasua kwa mradi huo pia kumetokana na baadhi ya watendaji wa serikali zote mbili kushindwa kwenda na “kasi ya kazi ya marais wa nchi zote mbili.”

Rais Magufuli amekuwa akiwalaumu watendaji wake katika mradi huo, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kwamba wamekuwa “goigoi.”

Taarifa zilizotufikia zinaeleza kuwa Rais Magufuli na mwenzie, Museveni wamekamia kuhakikisha uamuzi wa kuruhusu mradi mkubwa kuanza (FID) kwa bomba hilo na kupewa cheti haraka kabla ya mwaka huu, 2020 kuisha.