Walioandamana Hai walipangwa. Sabaya anamdanganya nani?

Inaonekana mzimu wa madiwani waliounga mkono juhudi za Rais John Magufuli unaanza kukitesa chama cha mapinduzi (CCM) wilaya ya Hai na mkoa wa Kilimanjaro.

Kikundi cha watu kama 200 kilipewa fedha ili tarehe 30 Julai 2020 kiandamane kwenda ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Hai, Bwana Lengai Ole Sabaya kupinga matokeo kura ya maoni kata ya KIA.

Tumeelezwa kuwa katika kata hiyo, Bwana Tehera Mollel aliongoza kura za maoni kwa kupata kura 78 akifuatiwa na Bwana Yohana Laizer kura 61 na Bwana Jullius Molllel 35.

Bwana Yohana Laizer alikuwa Diwani wa KIA kwa tiketi ya CHAD hadi 2018 alipotengenezewa kesi ya kumjaza mimba mwanafunzi na kupewa masharti ya kuhamia CCM kama anataka kesi hiyo ifutwe. Alifanya hivyo. 

Sasa katika kura za maoni za Udiwani Bwana Yohana Laizer ameshindwa na Bwana Tehera Mollel lakini DC Sabaya ambaye alishiriki kumnunua ile 2018, amesuka mpango ili watu waandamane kuonyesha kuwa Bwana Tehera Mollel hakubaliki.

Lakini, wamecheza sinema hiyo vibaya kwa vile kikanuni, waliopaswa kulalamika ni wagombea lakini wote waliridhika na matokeo hayo na hakuna aliyekata rufaa ndani ya siku tatu kama kanuni zinavyoelekeza.

Wakubwa ndani ya CCM wamekerwa na mchezo huo kwa kuwa wananchi wa kawaida hawawezi kuandamana kupinga matokeo ya kura za maoni zinazowahusu wana CCM kwa ngazi ya sasa.

Kingine kinachothibitisha DC Sabaya ana mkono katika vurugu zinazoendelea Hai ni watu hao kuandamana kwenda ofisini kwake badala ya kuandamana kwenda ofisi za chama cha Mapinduzi.

Taarifa tulizoletewa ni kwamba kuna nguvu kubwa ya fedha inatumika ili jina la Bwana Yohana Laizer lirudishwe na ionekane Bwana Tehera Mollel hakupatikana kihalali jambo ambalo si la kweli.

Kingine, cha kujiuliza ni kwanini walioandamana wanatoka kitongoji cha Palestina tu anachotoka Bwana Yohana Laizer, hili CCM na vyombo vya usalama vinapaswa kuchunguza mchezo huo mchafu.

Bahati mbaya sana tumeambiwa waandishi wengi wa habari wa mikoa ya Kilimanjaro na Arusha wamewekwa mfukoni na DC Sabaya na wanashiriki kuandika habari kwa kumpendezesha badala ya kuandika ukweli.