Tundu Lissu kupokwa pasipoti akitua Dar

Upo mpango uliosukwa kumnyang’anya pasi ya kusafiria Tundu Lissu mara atakapotua Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Lissu ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, ametia nia kugombea urais wa Tanzania katika Uchaguzi wa mwaka huu, 2020.

Lissu kutua nchini Julai 28, 2020

Vyanzo vyetu vya uhakika vinabainisha kuwa Lissu awali alitarajiwa kutua jijini Dar mnamo Julai 25, 2020 akitokea Brussels, Ubelgiji lakini kwa sababu zinazotajwa kuwa za kiusalama, amepangiwa kuwasili nchini Julai 28 ikiwa ni siku moja kabla ya vikao vikuu vya chama.

Taarifa za uhakika zinaonyesha kuwa Lissu atasafiri kwa ndege ya Qatar Airways – aina ya Airbus A319 akitokea Brussels hadi Frankfurt nchini Ujerumani na baadaye kuunganisha kwenda Doha, Qatar. Baadaye atapanda ndege ya Shirika hilohilo (Qatar Airways) aina ya Boeing 787-800 kuelekea Nairobi, Kenya na kisha kutua jijini Dar es Salaam. 

Pasi yake ya kusafiria kuchukuliwa

Uchunguzi wetu umebaini kuwa vyombo nyeti vya usalama vimejipanga kikamilifu na atakapotua wataichukua pasi yake ya kusafiria kwa kitakachodaiwa kuwa inahitajika na atarudishiwa baadaye.

Chanzo chetu kingine kimedokeza kuwa Lissu atakapowasili huenda akafikishwa mahakamani kwa tuhuma za kosa ambalo halitakuwa na dhamana.

Yeye, Lissu amenukuliwa akisema “Sina sababu ya kuamini kuwa nitazuiwa kurudi nyumbani, mimi si mhalifu kwani nilienda nje ya Tanzania nikiwa sina fahamu; nilishambuliwa kwa risasi mara 16 na watu ambao mpaka sasa hawajakamatwa”.

Kauli zake kumponza?

Mnyetishaji wetu amedokeza kuwa Serikali imekuwa ikirekodi kauli za Lissu alipokuwa akifanya ziara Ulaya na Marekani baada ya kupona na kwamba kauli zake zilikuwa zikiichafua nchi na kuitukanisha kimataifa.

Katika ziara yake, Lissu alizungumza na Watanzania wanaoishi Marekani, Uingereza na maeneo mengine, alizungumza zaidi namna Serikali inavyominya uhuru wa watu kujieleza, kuminya uhuru wa Vyombo vya Habari na ustawi wa vyama vya kiraia. 

Lissu kwa kauli zake pia anatuhumiwa kuwa amekuwa akichangia nchi kukosa au kupata kidogo misaada.

Kesi nne zinazomkabili mahakamani zatajwa kuchangia

Lissu ambaye alivuliwa ubunge wa Singida Mashariki na Spika Job Ndugai, anakabiliwa na kesi nne za uchochezi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam. Kesi hizo zote zilifunguliwa mwaka 2016.

Tayari Jeshi la Polisi limeweka wazi kwamba Lissu atakapotua Dar es Salaam atakamatwa na kuhojiwa kwa kile kinachoelezwa ni kwa tuhuma mbalimbali.

Lissu ambaye pia aliwahi kuwa mwalimu wa Shule ya Sekondari Bondeni, Arusha, alipigwa risasi 16 akiwa Dodoma bungeni na kufanyiwa upasuaji mara 24 akiwa nchini na nje; ikiwamo Kenya na Ubelgiji.