Njaa kwa Watia Nia CHADEMA: Kahangwa aondoa rufaa yake, afya yake yazorota

Mmoja wa wanachama wa CHADEMA aliyekata rufaa kupinga matokeo ya kura za maoni kwenye ubunge Jimbo la Karagwe mkoani Kagera, ameamua kuondoa rufani yake.

Mtia nia huyo, Deusdedith Kahangwa, juzi – Agost 7 aliandika barua (tumeinasa) kwenda kwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika akieleza kuondoa rufani yake kwa sababu za kudorora kwa afya yake.

Katika barua hiyo yenye nakala kwa mwenyekiti wa chama hicho na naibu katibu mkuu, inaeleza mengi lakini kubwa ni chama kushindwa kujipanga vyema kusikiliza rufaa za watia nia wenye kulalamika baadhi ya mambo katika mchakato wa kuwapata wagombea ubunge.

Taarifa zilizotufikia zinaeleza kuwa kudorora kwa afya ya mtia nia huyo ilichangiwa zaidi na njaa na kuzidiwa na usingizi.

Wakata rufani waliitwa Dar es Salaam ili kujieleza mbele ya kamati maalum, inayoongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe. Kikao kilifanyika Bahari Beach Hotel kuanzia mapema Agosti 5, na kiliendelea hadi alfajiri ambako malipo ya chama hicho kugharimia ukumbi yalikwisha, na chama kiliwaeleza walioitwa kwamba kikao kitahamia Makao Makuu, Kinondoni jijini Dar es Salaam ili kuendelea na mashauri.

Wote walioitwa katika kikao cha kusikiliza mashauri ya rufani, wengi wakitokea mikoani na hawakulipwa nauli wala posho, hivyo kushindwa kumudu gharama zaidi wakiwa Dar es Salaam.

Deusdedith, kama ilivyokuwa kwa wakata rufani wengine, walilia njaa na malazi kwa kuwa hawakupewa hata senti kuwawezesha kuishi kwa nafuu wakiwa Dar es Salaam.