Watia nia CHADEMA walia njaa. Hakuna posho wala nauli

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), leo kimeshindwa kulipa fedha ya siku moja kuendelea na kikao katika hoteli ya Bahari Beach, Kunduchi jijini Dar es Salaam.

Kikao hicho kilichoanza juzi, Agosti 5, 2020 katika hoteli hiyo, kilikuwa cha kumaliza migogoro ya uamuzi kwa watia nia 63 ambao walikata tufaa dhidi ya vikao vya chini.

Katika kikao hicho, wajumbe walialikwa kutoka maeneo yote ya nchi ambako kulikuwa na migogoro ya matokeo ya kura za maoni.

Wajumbe hao kutoka mikoa mbalimbali, walilazimika kukesha bila kula kwa kuwa hawakuwa katika utaratibu wa kulipwa posho wala nauli. Wote walitakiwa kujitegemea kufika Dar es Salaam na gharama zote za kuishi katika jiji hilo.

Taarifa zilizotufikia zinaeleza kuwa baada ya wajumbe kulalamika njaa, jana asubuhi kwa kukesha Bahari Beach, waliambiwa wajilipie kwenda kuendelea na kikao Makao Makuu ya chama hicho yaliyopo Ufipa, Kinondoni.

Kuondolewa kwa kikao hicho Bahari Beach,  kunadaiwa kutokana na kuisha kwa fedha ambazo chama kilitenga kwa kikao cha siku moja.

​Kwa kuwa kikao hicho kinaendeshwa kwa mfumo wa kimahakama, mlalamikaji na viongozi wa vikao, wote walitakiwa kuwepo ili kutolewa kwa uamuzi wa “busara.”

Baada ya kufika Makao Makuu, kikao hicho kiliendelea lakini wajumbe wengi walianza kulalamika kuhusu njaa na waliambiwa na viongozi wa chama hicho kwamba waendelee kuvumulia ili kumaliza mashauri hayo ya rufaa.

​Hata hivyo, hadi saa 7:00 mchana wa jana, bado walalamikaji 13 walikuwa bado wanasubiri kuhojiwa.

Hatua hii inaashiria chama hicho kikubwa cha upinzani, kina changamoto ya fedha, hasa katika kipindi hiki Tanzania ikijiandaa kuingia kwenye Kampeni za Uchaguzi Mkuu, zinazotarajiwa kuanza mwishoni mwa Agosti, 2020.