Zanzibar: Ulinzi waimarishwa; Vyombo vya Usalama vyajiandaa kukabiliana na lolote

Ulinzi, upekuzi, kuhojiwa kumeimarishwa zaidi katika bandari na uwanja wa ndege wa Zanzibar, ikiwa ni siku mbili  zikisalia kufika Oktoba 27, ili kuanza mchakato wa kupiga kura visiwani humo.

Kura za awali zitapigwa keshokutwa, Oktoba 27, 2020 kwa watumishi wa Idara za Usalama, Majeshi na Watumishi wa Tume ya Uchaguzi. Hii ni ili kutoa nafasi kwa watendaji hao kushiriki kikamilifu kutekeleza majukumu yao katika Uchaguzi siku inayofuata Oktoba 28.

Kazi ya kuhoji na kupekua kila anayekanyaga ardhi ya Zanzibar inafanywa na askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), Uhamiaji na Kikosi Maalum kutoka Idara ya Usalama.

Imedokezwa kuwa maofisa hao ni kutoka Vyombo vya Usalama vya Tanzania Bara na kwamba wapo wanaoficha sura zao kwa soksi-uso (face masks).

Aidha, wanausalama hao wote wanavaa nguo za kijeshi, wakiwa na silaha za kivita huku wengine wanaovaa kiraia wakiwa na pistol.

Chanzo chetu kimetembelea bandarini na Uwanja wa ndege wa Zanzibar na kukutana na “karinyekarinye” ya upekuzi na maswali kwa kila mtu anayeingia visiwani humo.

Mbali na kuwepo maeneo hayo, wanajeshi wanaonekana kurandaranda mitaani katika maeneo mengi ya Zanzibar wakiwa na silaha za moto. Idadi kubwa wakionekana kuwepo Kisonge, Mkwajuni, Mlandege na Mnazi Mmoja.

Katika eneo la Kisonge jana, barabarani kulikuwa na kundi la wanajeshi ambalo lilikuwa likikamata na kuhoji vijana waliokuwa wakitembea kwa makundi na kuwalazimisha kuruka kichura-chura kabla ya kuwaamuru kutawanyika, kila mmoja akiondoka lwake, bila kufuatana.

Hali ya Usalama katika visiwa hivi ni tete kwa kuwa zipo hisia za kutokea vurugu siku ya kupiga kura au baada.