Zanzibar: Mazrui atekwa, Maalim Seif kutoa kauli nzito leo

Mgombea urais Zanzibar kupitia ACT-Wazalendo,  Maalim Seif Shariff Hamad, leo anatarajiwa kutoa amri kwa wanachama na mashabiki wake kwenda vituo vya kupigia kura Oktoba 27, ili kuzuia kile anachoita “wizi wa kura na mbinu chafu kuvuruga uchaguzi.”

Taarifa tulizopata asubuhi ya leo zinaonyesha kuwa Maalim Seif katika mkutano wake unaofanyika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Zanzibar, atawaamuru wafuasi wake kufanya hivyo bila “kuogopa lolote wala chochote.”

Jumanne, Oktoba 27, 2020 ni siku ambayo Maofisa wa Idara za Usalama na Watumishi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar kupiga kura ili kupata nafasi ya kusimamia mchakato wa kupiga kura kwa umma siku inayofuata. 

Taarifa zinaeleza kwamba Maalim Seif na chama chake wana hisia kuwa Tume, Idara za Usalama na Chama Cha Mapinduzi (CCM) watatumia muda huo kuvuruga kura kwa kuweka idadi kubwa ya kura katika masanduku ili kuhakikisha ushindi kwa Dk. Hussein Mwinyi, mgombea urais wa chama tawala.

Kiongozi mmoja wa juu wa ACT-Wazalendo amesikika muda huu akieleza kwamba chama chake hakitakubali kudhulumiwa ushindi kwa njia za ujanjaujanja, ikiwamo kuongeza idadi ya kura kupitia kile anachoita – “njia haramu za CCM na Serikali yake.”

Asubuhi ya leo, Naibu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Nassor Mazrui anadaiwa kutekwa na vyombo vya Usalama ambapo chama chake kimesema tukio hilo lilitokea baada ya Gari lake kugongwa katika eneo la Kikosi Cha JKU Saateni, akiwa njiani kuelekea ofisi za chama zilizopo Vuga.

Tayari maeneo ya Mnazi Mmoja na mitaa jirani kuna idadi kubwa ya wanajeshi na askari kanzu wakivinjari. Wapo wanaotembea na wengine wakionekana kwenye magari.