Zanzibar: Kura 40,000 nje ya utaratibu zaandaliwa kupitia kura ya awali

Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Chama Cha Mapinduzi (CCM) na taasisi nyeti za serikali wanadaiwa kupanga kuhakikisha kura 40,000 zinapatikana siku moja kabla ya tarehe rasmi ya kupiga kura, Oktoba 28, 2020.

Zanzibar imepanga kwa watumishi wa majeshi, idara za usalama na watumishi wa ZEC, kupiga kura Oktoba 27 ili kuwapa nafasi kutekeleza majukumu yao siku rasmi ya uchaguzi. 

Uchunguzi wetu umebaini kwamba ushirika huo umeweka mikakati ya kupata idadi hiyo ya kura kwa mgombea wa CCM, kwa nafasi ya urais wa visiwa hivyo, Dk. Hussein Mwinyi wakilenga watumishi kupiga kura tatu au zaidi ili kufika idadi inayotakiwa.

Mmoja wa waratibu wa mpango huo haramu amebainika kuwa ni ndugu Julius Haule ambaye ni mwanausalama kutoka Tanzania Bara, aliyesikika akisema kamwe mgombea wa CCM hawezi kushindwa, “lije jua, inyeshe mvua.”

Vyanzo vyetu vinaonyesha “wajumbe” wa ushirika huo walikutana Oktoba 9, mjini Zanzibar katika moja ya Ofisi za Serikali na kufikia uamuzi huo baada ya kuwepo ripoti zilizoonyesha mgombea wa CCM atashindwa ikiwa “haki bin haki” – kupitia sanduku la kura, itasimama.

Mipango hii endapo itatekelezwa, huenda ikaiingiza Zanzibar katika machafuko makubwa.

Katika uchaguzi wa mwaka huu, Zanzibar imeandikisha na kuhakiki wapigakura 566,352.