Mtego kwa Lissu? Serikali yawawekea ngumu Wadhamini kujiondoa kwenye kesi

Serikali imeamua kula matapishi yake baada ya leo kubadili msimamo wake kumkamata Tundu Lissu atakaporejea nchini.

Katika mahakama ya Kisutu, Serikali kupitia wakili wake mwandamizi, Simon Wankyo imeieleza mahakama itupilie mbali maombi ya wadhamini wake, Robert Katula na Ibrahim Ahmed wanaotaka kujiondoa udhamini kwa Lissu katika kesi ya jinai inayomkabili.

Serikali kupitia hati kinzani dhidi ya maombi ya wadhamini hao, inaeleza kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam haina mamlaka ya kisheria kutoa uamuzi juu ya maombi hayo. Hivyo yatupwe.

Lissu katika kesi hiyo namba 208 ya mwaka 2016, anakabiliwa na jinai ya uchochezi pamoja na mmiliki wa gazeti la Mawio, Simon Mkina, Jabir Idrisa ambaye ni mhariri wa gazeti hilo la uchunguzi na mchapishaji, Isamail Mahboob.

Februari, mwaka huu, wadhamini wa Lissu katika kesi hiyo waliomba mahakama iwaruhusu kujiondoa udhamini kwa madai ya kukosa ushirikiano kutoka kwa mshitakiwa Lissu.

Tangu kipindi hicho, Serikali kupitia kwa mawakili wake imekuwa ikiomba mahakama kutoa hati ya kukamatwa Lissu, hatua ambayo mahakama imekuwa ikitupilia mbali maombi hayo.

Kumbukumbu za kimahakama zinaonyesha kuwa serikali imetoa maombi ya kukamatwa Lissu mara tano. Mara zote mahakama inayakataa kwa hoja kwamba wadhamini wake wapo.

Lissu ambaye alivuliwa ubunge wa Singida Mashariki na Spika wa Bunge, Job Ndugai kwa madai ya utoro, aliondolewa nchini, bila kujitambua mwaka baada ya kushambuliwa na wale wanaotajwa na serikali kuwa ni “watu wasiojulikana” wakati akitoka bungeni jijini¬† Dodoma tarehe 7 Septemba mwaka 2017.

Taarifa zinaeleza kuwa Lissu alimiminiwa mvua ya risasi 36 akiwa ndani ya gari lake na 16 ziliingia mwilini mwake, hasa maeneo ya mguu wa kulia, kiuno na mkono.

Mwanasiasa huyo kufuatia shambulizi hilo, amefanyiwa upasuaji mara 24. Upasuaji huo ulifanywa katika Hospitali ya Nairobi, Kenya na baadaye Hospitali ya Chuo kikuu cha Leuven, Ubelgiji.

Wiki mbili zilizopita tulieleza kuwa Lissu angerejea nchini Julai 28, mwaka huu na kufichua mipango ya kumkamata akiwa Uwanja wa Ndege.

Lissu ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, ametangaza nia kuwania kuteuliwa na chama chake kugombea urais wa Tanzania katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.