Mangula aomba kupumzika CCM. Uzee, changamoto ya Afya vyachangia

Makamu wa Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula ameomba kupumzika kazi hiyo baada ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.

Barua aliyoandika Juni 22, 2020 kwenda kwa Mwenyekiti wake, John Pombe Magufuli, inaeleza kuwa anaomba kupumzika kutokana na kuwa na umri mkubwa na changamoto  za afya. Hivi sasa Mangula ana miaka 79.

Uchunguzi wetu unaonyesha kuwa Mangula aliomba kupumzika mapema zaidi, lakini Magufuli alimkatalia na kumuomba asubiri hadi Uchaguzi Mkuu utakapomalizika.

Mangula alimweleza kwa mara ya kwanza Mwenyekiti wake alipokwenda kumjulia hali baada ya kupata ahueni kuwa angependa kupumzika, lakini Magufuli alisema “subiri kwanza upone tuzungumze.”

Mangula ambaye hupenda kuitwa “mzee wa mafaili” na Rais Magufuli, alikumbwa na maradhi ambayo hayakuwekwa wazi, lakini yaliyochagizwa zaidi na kulishwa sumu.

Taarifa kutoka ndani ya Jeshi la Polisi ya Machi 9, 2020 ilieleza kuwa Mangula alipewa na hatimaye kula (kunywa?) sumu iliyosababisha kudondoka wakati akiendelea na kikao cha CCM, Dar es Salaam kilichofanyika Februari 28, 2020.

Tangu kuanguka na kulazwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es  Salaam na baadaye kuhamishiwa mahali ambako hakujawekwa wazi, Mangula aliuguzwa kwa miezi takribani mitatu. Aliibuka hadharani Mei, 2020.

Mangula aliyewahi pia kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, amekuwa nguzo muhimu kwa uhai wa chama hasa kipindi cha Mwenyekit John Magufuli na Katibu Mkuu mpya, Dkt. Bashiru Ally ambaye alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Taarifa zinaeleza kuwa Rais Magufuli alipenda kufanya kazi na Mangula ili kuwapa ushauri wa namna njema ya kuongoza chama, kazi ambayo ingekuwa ngumu zaidi kwa viongozi wote wa juu kuwa “wageni.”