Dkt. Mwinyi akumbana na vizingiti Zanzibar

Shamrashamra na makeke ya kisiasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar yameshindwa kuonekana katika vijiwe maarufu vya mashabiki wa chama hicho – maskani, baada ya Dkt. Hussein Mwinyi kuteuliwa kuwania urais wa visiwa hivyo.

Vijiwe maarufu kikiwemo Kisonge, maeneo ya Michenzani, Zanzibar, hakuonekani kuwa na uhai tangu kutangazwa kwa Dkt. Mwinyi jijini Dodoma mwishoni mwa wiki.

Katika mbao maarufu za ‘amsha-amsha’ za Kisonge, hakukuwepo maandishi yoyote ya kupongeza uteuzi wa Dk. Mwinyi hadi Jana asubuhi, ikiwa ni siku mbili baada ya Mkutano Mkuu wa chama hicho tawala uliofanyika Dodoma.

Hata hivyo, taarifa za mchana huu wa Leo- Julai 14, zinaeleza kuwa baadhi ya vijana wa CCM wameandika mstari mmoja kwa maneno matatu tu; Ahhh! Hongera Dkt. Mwinyi.

Ifahamike kwamba katika kipindi kama hiki miaka ya nyuma na hasa katika vuguvugu la uchaguzi tofauti na mwaka huu, Kisonge na ndiyo mzizi wa amsha-amsha. Mbali na Kisonge, maeneo mengine yenye vijiwe, ikiwemo Mkunazini na Miembeni kunaonekana kupoa.

Wachambuzi wa siasa za Zanzibar wanasema kwamba kuchaguliwa kwa Dkt. Mwinyi “kumewaduwaza,” kwani hawakuamini.

Inadaiwa kuwa chaguo la wanachama wengi wa Zanzibar, hasa wale wanaoingia kwenye vikao vya uamuzi, ni Shamsi Vuai Nahodha.

Wengi wa wahafidhina wa CCM Zanzibar wanaeleza kwamba Dkt. Mwinyi siyo chaguo lao, bali ni la Rais John Magufuli na wajumbe wengine wa Kamati Kuu ya chama chao.

Wanaeleza kwamba Machi, mwaka huu, Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ali aliwaeleza wajumbe wa vikao vya chama hicho Zanzibar, kwamba Rais Magufuli anapenda kufanya kazi na Dkt. Mwinyi.

Baada ya kauli hiyo, wajumbe wengi hawakuridhika na kuanza kujipanga, hata hivyo, wanadai walizidiwa “kete” na idadi kubwa ya wajumbe kutoka Tanzania Bara.