Mhariri wa Gazeti la HabariLeo alipokea rushwa toka Kamal Steel Ltd

Kampuni iliyofichwa na TAKUKURU baada ya kumkamatisha rushwa mhariri wa gazeti la Kiswahili la Serikali, HabariLeo, Oscar Mbuza, imebainika kuwa ni Kamal Steels Limited iliyo na ofisi zake Kitalu namba 188/2, Barabara ya Mwakalinga eneo la viwanda Chang’ombe – Temeke, Dar es Salaam.

Katika taarifa yake kwa umma kuhusu kukamatwa kwa Mhariri huyo iliyotolewa Juni 30, 2020, TAKUKURU ilificha jina la kampuni hiyo huku ikieleza kwamba uchunguzi ulikuwa umekamilika.

Uchunguzi wetu umebaini kuwa Oscar aliomba kupewa rushwa ili asiandike kuwepo kwa watumishi kutoka India wasiokuwa na vibali vya kufanya kazi nchini.

Vyanzo vyetu vimebaini kuwa mmoja wa watumishi hao wawili aliajiriwa idara ya fedha, akiwa anaishi na kufanya kazi kwa miaka mitatu sasa. Inaelezwa kwamba mtumishi huyo kibali chake cha kwanza kiliisha tangu Oktoba 2019. Sheria za Tanzania haziruhusu wageni kupata ajira bila kuwa na vibali.

Mhariri huyo alikamatwa akiwa amepokea kitita cha Sh 1,500,000 ikiwa ni sehemu ya rushwa waliokubaliana na Meneja Utumishi wa kampuni ya Kamal. Makubaliano yalikuwa ni Oscar kupokea jumla ya Sh. 6,000,000, lakini kumbe mtego ulitegwa ili kumkamata.

Mhariri huyo anayesoma Shahada ya pili katika Chuo Kikuu cha Kampala, alifikishwa Mahakama ya Wilaya ya Temeke na kusomewa mashitaka yake. Alipewa dhamana.