Mizengwe: Bilioni 425 za Mwekezaji zazuiliwa Tanzania, Kenya yamshawishi ahamie kwao

WAWEKEZAJI na matajiri wa viwanda katika nchi kadhaa duniani, familia ya Jamal Hassan Abdullah Alawadhi ya Kuwait, wamekumbana na mkwamo wa kuanzisha kiwanda cha dawa nchini Tanzania baada ya kuleta nchini kiasi cha Euro 150,000,000 ambazo ni takribani Shilingi za kitanzania bilioni 425, ambazo bado zinadaiwa kushikiliwa na serikali kwa zaidi ya miaka miwili sasa.

Chanzo

Familia ya matajiri hao iliingia ubia na kampuni ya wazawa (Watanzania) ya Pharmaceutical Investment Limited (PIL) ambayo ilinunua asilimia 60 ya hisa za kiwanda cha Serikali cha kutengeneza dawa cha Tanzania Pharmaceutical Industries Limited (TPI) kilichopo Arusha. Serikali ya Tanzania ilibaki na asilimia 40 ya hisa.

Aidha, inaelezwa kuwa baada ya kukamilika kwa mchakato wa awali wa kununua hisa, hatimaye mwekezaji aliridhika na kuamua kuwekeza fedha katika kiwanda hicho, makubaliano yakiwa matengenezo yakamilike haraka na uzalishaji wa dawa uanze mapema kadri inavyowezekana.

Kiasi hicho cha fedha kilitumwa nchini na kupokelewa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) mnamo Septemba 12, 2018, ikiwa ni mtaji wa kuanzisha kiwanda hicho cha dawa muhimu kwa matumizi ya binadamu.

Baada ya BoT kupokea kiasi hicho cha fedha, ilitakiwa kuingizwa kwenye akaunti ya PIL iliyoko Benki ya CRDB, tawi la Holland House, Dar es Salaam ili matumizi yake yaanze mara moja kwa kiwanda kuanza uzalishaji.

Mkwamo

Hadi leo, ikiwa ni miaka miwili na miezi miwili, bado kiasi hicho hakijaingizwa kwenye akaunti za wahusika. Sababu; haziko wazi, ingawa inawezekana kuna baadhi ya maofisa Serikalini bado wanaendelea na mchakato wa kujiridhisha kuhusu vyanzo vya fedha hizo.

Mmoja wa wanafamilia ya Jamal Alawadhi ameongea na mwandishi wa habari hii kuhusu uhalali wa fedha hizo za uwekezaji na amekiri kwamba amewahi kuhojiwa na kuombwa nyaraka kadhaa zinazoonyesha vyanzo vya fedha zake.

Anasema katika vikao walivyofanya na uongozi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na BoT, Serikali iliridhika kuwa fedha hizo ni halali na kwamba wakati wowote zingeweza kuingia kwenye akaunti ya kampuni ya PIL.

“Jamal amekuja Dar es Salaam mara nyingi na kuwa na vikao na viongozi wa TIC, na hakuna wasiwasi wowote juu ya uhalali wa kipato chake binafsi wala cha familia yetu, tunafanya biashara halali na mara nyingi tuko kusaidia jamii,” anaongeza mwanafamilia huyo.

Rais Magufuli ahusishwa kuokoa jahazi

Hata hivyo, pamoja na ahadi hiyo ya BoT ya fedha kuingizwa kwenye akaunti yao, bado dalili za kuanza kazi ya kukifufua kiwanda zilikuwa finyu, hivyo uongozi wa PIL uliamua kuandika barua kwa Rais John Magufuli – Januari 15, 2019 kumjulisha juu ya jambo hili na pia kuomba msaada wake ili kuhimiza utekelezaji wake.

Taarifa tulizo nazo zinaonyesha kwamba Ikulu ilijibu barua hiyo siku – Januari 16, kwa simu ikieleza kwamba uongozi wa PIL unatakiwa kuonana na Mkurugenzi Mkuu wa TIC ili kufikia muafaka.

Kilichotokea TIC

Januari 17, 2019, uongozi wa PIL, ulifika ofisi za TIC na kukutana na Mkurugenzi Mkuu, Geoffrey Mwambe (hivi sasa hayupo tena) ambaye kwa mujibu wa maelezo ya wawekezaji hao, aliwapa ushirikiano na kuwaeleza kwamba suala lao litamalizika karibuni.

Katika mkutano na Mwambe, PIL ilitakiwa kuonyesha muhtasari na mchanganuo wa fedha hizo zitakavyotumika, uhalali wake (kwa mara nyingine) na kuomba wawekezaji wote, ikiwemo familia ya Alawadhi kufika nchini kukutana na “mamlaka zinazohusika.”

Siku 10 baada ya kumalizika kwa kikao hicho, mmoja wa wanafamilia ya Alawadhi, Eng. Jamal aliwasili nchini na siku iliyofuata, Januari 28, 2019, akiwa amefuatana na wanahisa (Watanzania) walifanya kikao na Mwambe, jijini Dar es Salaam na kukubaliana kukutana baada ya siku mbili ili kukamilisha mazungumzo hayo.

Inaelezwa kuwa Januari 30, 2019, Eng. Jamal na wanahisa wengine walifika TIC na kufanya kikao ambacho kilichukua muda mrefu huku Mwambe akiwaambia wawekezaji hao “wasiwe na wasiwasi,” kwani suala lao limekamilika.

Baada ya kumalizika kwa kikao hicho, Eng. Jamal alilalamikia uwepo wa vikao vingi huku akionyesha kutokujua lini kiwanda kingeanza uzalishaji.

Mwekezaji akata tamaa, ashawishiwa kuhamia Kenya

Taarifa zinaeleza kwamba Eng. Jamal ametishia kuondoa fedha zake ikiwa ataendelea kupewa ‘ahadi’ ambazo zinachelewesha kuanza kwa uzalishaji wa dawa.

Uchunguzi wa awali unaonesha kuwepo kwa madalali kutoka Kenya wanaomshawishi Eng. Jamal kupeleka fedha hizo nchini kwao ili kiwanda hicho kijengwe haraka.

“Jamal amefuatwa na Wakenya, wanaomba akawekeze kwao, lakini amesema bado hana nia hiyo, lakini ikiwa atashindwa kabisa itabidi aondoe fedha zake na kwenda huko,” anasema mwanafamilia.

Imebainika kwamba Wakenya hao aliokutana nao Dar es Salaam, wameahidi kumpa eneo kubwa la uwekezaji huko Mombasa au mahali anapopenda ili kuanza ujenzi wa kiwanda na kuwa atapewa fursa ya kipekee katika utekelezaji wa uwekezaji wake.

Mkuu Mpya wa TIC anena

Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Maduhu Kazi akizungumzia suala hilo, amesema wahusika wa uwekezaji huo wafike ofisini kwake ili kuona ni wapi wamekwama na kuchukua uamuzi wenye manufaa kwao na Tanzania na watu wake.

Kazi amesema ofisi yake iko wazi na kwamba haina kikwazo kwa mwekezaji yeyote ikiwa atafuata na kutimiza masharti na matakwa ya kisheria ya uwekezaji na kwamba uamuzi ikiwa kila kitu kimekamilishwa, utatolewa kwa muda mfupi.

Rais Magufuli na ahadi ya kuboresha mazingira ya uwekezaji

Katika hotuba yake bungeni, Dodoma, wakati wa kulifungua Bunge baada ya kutangazwa mshindi wa urais kwenye Uchaguzi wa Oktoba 28, 2020, Rais Magufuli alitangaza uamuzi wake kuweka TIC chini ya Ofisi ya Rais.

Alisema hatua hiyo ina nia ya kuharakisha uamuzi kwa wawekezaji makini, kwani Tanzania inahitaji zaidi uwepo wa wawekezaji ili kuimarisha uchumi wake unaoendelea kukua.

Faida za kiwanda kujengwa Tanzania

Ikumbukwe kuwa kuanza kazi ya uzalishaji wa dawa hizo muhimu, kungepunguza zaidi gharama za kuagiza Dawa kwa Serikali na kuokoa zaidi ya Shilingi bilioni 900 zinazotumika kila mwaka kuagiza dawa nje ya nchi.

Mbali na kuokoa fedha, kiwanda hicho kingeongeza ajira kwa Watanzania na kupunguza kadhia ya ukosefu wa ajira.

Mbali na faida hizo, kiwanda hicho kingekuwa chanzo kikubwa cha kodi ambayo ingekuwa chachu ya maendeleo kwa kuwezesha kuwepo kwa barabara, ujenzi wa shule na hata hospitali.