Ofisi ya Spika ‘kuwalinda’ wabunge wa Viti Maalum wa CHADEMA

Ofisi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejiandaa kulinda usalama wa Wabunge wa viti maalum wa CHADEMA dhidi ya tuhuma na hata vurugu wanazoweza kufanyiwa na yeyote.

Msimamo huo umetolewa faragha jana na Spika Job Ndugai kwa wabunge hao aliokutana nao ofisini kwake Dodoma.


Taarifa za uhakika zinaeleza kuwa hata kama wabunge hao wataitwa na chama chao kuhojiwa kwa lolote, ofisi ya Spika itabidi ibariki mwito huo.

Hatua hiyo inafuatia kuwepo sintofahamu ndani ya chama hicho cha upinzani kuhusu hatma ya nafasi za wabunge wa viti maalum baada ya kupata zaidi ya asilimia tano za kura za Urais.

Kumekuwepo na minyukano ya maneno miongoni mwa viongozi wa chama hicho na kujenga kambi mbili; moja ikiona umuhimu wa wabunge kuhudhuria vikao na jingine likiona kuingia bungeni ni kuhalalisha kile CHADEMA wanaita “uharamia na wizi wa ushindi wao.”

Jana viongozi 19 waandamizi wanawake wa chama hicho waliapishwa na Spika Ndugai kuwa wabunge rasmi wa kambi ya upinzani. Hatua ambayo imezua taharuki ndani ya chama, huku wengi wakiwaeleza kuwa ni wasaliti.

Tayari Katibu Mkuu wa CHADEMA, leo amewaambia waandishi wa habari kwamba chama hicho hakijapeleka majina ya wanawake wa viti maalum na hao walioapishwa ni “wabunge haramu.”