Tanzania bado inaendelea kuficha taarifa za maambukizi ya virusi vya Corona, hata hivyo vifo vinavyotokana na ugonjwa huo vinaiumbua.
Taarifa za kitabibu na maabara tulizo nazo zinaonyesha ugonjwa huo bado upo na usiku wa kuamkia jana “changamoto ya upumuaji” imeuchukua uhai wa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Tabora, Salvatory Bongole.
Uchunguzi wetu katika Hospitali ya Mkoa wa Tabora, Kitete umebaini kuwa Jaji Bongole alifariki muda mfupi baada ya kufikishwa hospitalini hapo saa 5:32 usiku.
Imebainika kuwa Jaji Bongole alikuwa na matatizo ya upumuaji kwa zaidi ya wiki mbili, akiwa nyumbani kwake, lakini hakwenda hospitali kwa matibabu zaidi.
Taarifa uhakika kutoka ndani ya familia yake zinaeleza kuwa Jaji Bongole alihisi kuwa na dalili zote za maambukizi ya COVID-19, lakini aliamua kuanza matibabu mbadala yaliyohamasishwa na serikali ya Rais Magufuli, ikiwamo kujifukiza (kupiga nyungu).
Pamoja na kujifukiza, Jaji Bongole alijaribu kutumia dawa kadhaa zilizoibuka maeneo mengi ya Tanzania zikielezwa kutibu Corona.
Jaji Bongole inaelezwa kuwa alianza kujifukiza mwishoni mwa wiki ya kwanza ya mwezi huu, Julai huku akihimiza vijana wa familia yake kufanya hivyo ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona.
Familia ya Bongole ambao ni watu kutoka mkoani Tabora na makazi yake yaliyoko Bunju, Dar es Salaam inaeleza kuwa jaji huyo mfawidhi huenda alipata maambukizi hayo kutoka kazini au kanisani kwake, Katoliki ambako hakuacha kwenda wala hakuwa “muumini wa kuvaa barakoa.”
Mazishi ya Jaji Bongole yanatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam ambako ndiko makazi ya familia yake yapo.
Taarifa za COVID-19 nchini bado kizungumkuti
Tanzania iliripoti kuwa na mgonjwa wa kwanza wa maambukizi hayo nchini Machi 16 na kuanza kutoa taarifa kwa umma na dunia, lakini baada ya siku 49, iliacha kutangaza kasi ya maambukizi, idadi ya wagonjwa, waliopona na hata vifo.
Tangu Tanzania ilipoacha kutangaza taarifa za takwimu za ugonjwa huo, imekuwa ikilalamikiwa na kubezwa na mataifa mengine na taasisi za afya za dunia kwamba haiko makini katika mapambano ya ugonjwa huo unaoaminika kuanzia huko Wuhan, China mwishoni mwa mwaka jana.
Shirika la Afya Duniani linaendelea kusisitiza kuwa ugonjwa huo hadi sasa hauna tiba wala chanjo, hivyo watu wanahimizwa kuchukua tahadhari ikiwa ni pamoja na kunawa mikono kwa sabuni na maji yanayotiririka, kuziba mdomo wakati wa chafya, kuvaa barakoa, kutumia vitakatisha mikono na kuacha kuzurura.
Leave a Reply