Paul Makonda amejaa Kiburi na Uthubutu usiomithilika

Uamuzi wa Paul Makonda kuacha ukuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na kwenda kuomba ridhaa ya chama chake kugombea ubunge, unachambuliwa kwa namna mbili kuu: Amejaa kiburi au kuwa na uthubutu usiomithilika.

Tayari Makonda amechukua fomu ya kuwania ubunge Jimbo la Kigamboni, Dar es Salaam na ameirejesha leo.

Kumekuwepo na hisia tofauti juu ya uamuzi huo wa Makonda, wachambuzi wa siasa na wananchi wakieleza mengi juu ha uamuzi wake.

Wapo wanaomuona Makonda kuwa ni kijana aliyejaa kiburi cha uongozi kwa kuwa anaonekana kukaidi maono na msimamo wa viongozi wa juu wa chama chake, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhusu wateule wa Rais John Pombe Magufuli kukimbilia ubunge.

Wapo pia wanamuona anathubutu zaidi ya wanasiasa wengi vijana katika kuchukua uamuzi bila kujali athari zake baadaye.

Hisia hizi zinafuatia msimamo wa Mwenyekiti wa CCM, Rais Magufuli na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Bashiru Ally ambao wote kwa nyakati tofauti wamekuwa wakisisitiza vijana kuridhika na nafasi zao.

Tangu mwaka jana, 2019 Rais Magufuli katika mikutano ya hivi karibuni amekuwa akiwaasa wateule wake kuacha kukimbilia kuomba ubunge wakati amewapa nyadhifa kubwa kuwatumikia wananchi.

Naye Dk. Bashiru, bila kupepesa macho akiwa na mkutano Kigamboni mapema mwezi huu, alitamka kwamba Makonda asikimbilie ubunge katika Uchaguzi wa mwaka huu, kwani bado ana umri mdogo, hivyo kuwa na nafasi nzuri zaidi kwenye siasa siku za usoni.

Hata hivyo, pamoja na maono na ushauri wa viongozi wake, Makonda ameamua kuchukua fomu Kigamboni.

Makonda amenusa hatari mbele?

Wachambuzi wa siasa wanaeleza kuwa Makonda pia huenda amepiga hesabu zake kisiasa na kubaini ukakasi baada ya kumalizika Uchaguzi Mkuu baadaye mwaka huu.

Ukakasi unaoelezwa na wachambuzi hao ni “kutemwa” katika nafasi ya ukuu wa mkoa, baada ya kuwa na tuhuma nyingi katika utendaji wake.

Makonda katika uongozi wake amekumbwa na kashfa ya kuvamia ofisi za chombo cha habari, Clouds Media Group, kutukana na kukejeli watu, kutuhumu na kukamata watu, wengine bila ushahidi, kwamba wanafanya biashara ama kutumia dawa za kulevya na pia akielezwa kutumia madaraka yake vibaya.

Hata hivyo, pamoja na tuhuma hizo, ikiwamo ile iliyoelezwa na Marekani kwamba “anaminya haki ya wengine kuishi,” hata kumwekea zuio la kuingia nchini humo, Makonda hajapewa adhabu yoyote iliyowekwa hadharani na aliyemteua au taasisi nyingine zenye mamlaka kufanya hivyo.