Sheikh Ponda anaendelea kushikiliwa na Polisi – Siku ya 8

Katibu Mkuu wa Shura ya Maimamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda aliyekamatwa na Jeshi la Polisi siku nane zilizopita (Julai 9, 2020) yuko Kituo cha Polisi Magomeni jijini Dar es Salaam.

Vyanzo vyetu vya uhakika vimebainisha kuwa Ponda alihamishiwa kituoni hapo juzi usiku akitolewa Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar.

Hata hivyo, uwepo wa Sheikh huyo katika kituo hicho umekuwa ukifanywa siri kubwa bila kuelezwa sababu za kufanya hivyo.

Ahamishwa vituo huku akiendelea kuhojiwa

Taarifa tulizozipata jioni ya leo zinaeleza kuwa Sheikh Ponda amekuwa akihamishwa kituo kimoja hadi kingine lakini akipelekwa Kituo Kikuu kwa ajili ya kuhojiwa kila alfajiri.

Inaelezwa kuwa sababu za kufanya hivyo ni kuhakikisha kuwa uwepo wake katika kituo kimoja cha Polisi haufahamiki haraka.

Sababu za kumshikilia hadi sasa kwa mujibu wa Polisi ni kuwa wanaendelea kumhoji kuhusu waraka alioutoa kwa umma, ukielezwa na Serikali kwamba “umejaa uchochezi.”

Kufikishwa Mahakamani Julai 21, 2020

Tunazo taarifa zinazoonyesha kuwa wiki ijayo, Jumanne, Julai 21, Sheikh Ponda atafikishwa Mahakama ya Kisutu akikabiliwa kwa makosa ya uchochezi.

Kiongozi huyo alikamatwa na polisi maeneo ya Ilala Bungoni, Dar es Salaam wakati akitoka msikitini kwa swala ya alasiri na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi na hadi sasa hajaachiwa huku ikidaiwa kuwa mwanasheria na ndugu zake hawajajulishwa alipo.

Watumiaji wa Mitandao ya kijamii wamekuwa wakihoji alipo kiongozi huyo na idadi kubwa ya watu wamekuwa wakitaka afikishwe mahakamani.

Sheria za Tanzania zinaelekeza kuwa Jeshi la Polisi linapomkamata mshukiwa wa kosa lolote anapaswa kuachiwa huru kwa dhamana ya jeshi hilo au kufikishwa mahakamani ndani ya saa 24 tangu kukamatwa kwake.