Heshima, hadhi na uaminifu kwa Vyombo vya Habari, hasa magazeti kwa sasa inaelekea kukoma baada ya wamiliki, waandishi waandamizi na wahariri kuhamia kwenye siasa.
Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, 2020 umedhihirisha hivyo baada ya Viongozi hao wa Vyombo vya Habari kukimbilia kuomba kuteuliwa na Vyama vya Siasa ili kugombea nafasi za ubunge.
Kwa uhakika, mwanzoni mwa mwezi huu tuliandika kuhusu kuondoka kwa Francis Nanai, aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Magazeti ya The Citizen, Mwananchi na Mwanaspoti kwenda kugombea ubunge Jimbo la Busega. Nanai ni mwanachama wa CCM tangu akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Aidha, mwandishi mwandamizi na mmoja wa Wakurugenzi wa Gazeti la kila wiki la Jamhuri, Manyerere Jackton naye anatarajiwa kusaka uteuzi wa CCM ili agombee Ubunge Jimbo la Butiama.
Mwandishi mwingine ambaye tuna taarifa za uhakika ni Khamis Mkotya ambaye anatarajiwa kuomba chama chake cha CCM kumteua kugombea Jimbo la Chemba. Huyu anatangaza nia ikiwa ni mara ya pili.
Ni wazi kuwa waandishi hawa wamekuwa wakipendelea chama chao katika kutekeleza majukumu yao na bayana pia kuwa wamekuwa wakiandika habari ambazo aidha waliziandika kishabiki au kwa maelekezo maalum.
Wachambuzi wa mambo ya habari kadhaa ambao tumeongea nao wameeleza kusikitishwa kwao na hatua hii ya waandishi wakieleza inaharibu zaidi uaminifu wa vyombo vya habari kwa wasomaji jambo ambalo wamedai ni hatari kwa ustawi wa tasnia ya habari.
Imeelezwa kuwa hata kushuka kwa mauzo ya magazeti na usikilizaji wa vyombo vya habari kumechangiwa zaidi na wahariri waliokuwa wakiruhusu habari za kupendelea vyama vyao hasa chama tawala.
Kumekuwepo na wimbi kwa watendaji wa Vyombo vya Habari kuacha kazi zao na kufukuzana na uteuzi wa nafasi za Ukuu wa Wilaya, Ukurugenzi wa Halmashauri au u-Katibu Tawala. Ni katika kufukuzana huko, habari nyingi zilikuwa zikionekana kupendelea CCM huku wengine wakithubutu kuwatukana wapinzani waziwazi na baadae kuteuliwa baada ya ‘kazi nzuri’.
Mwanzoni, ilionekana kama uongozi wa Rais Magufuli umepunguza kuwabeba waandishi wanaojipendekeza lakini teuzi za hivi karibuni zinaonyesha tofauti. Wanaotangaza nia kwa sasa inadaiwa wamedokezwa kuwa lazima waonekane waliingia kwenye kinyang’any’iro ili waweze kukumbukwa kwenye teuzi za kuanzia mwaka 2021.
Leave a Reply