Uteuzi wa urais unapohuisha ndoa; Mkapa na Dkt. Hussein Mwinyi

Huenda historia ya kuimarisha ndoa za wagombea urais Tanzania ikajirudia katika mchakato wa Uchaguzi mwaka huu, 2020.

Ilikuwa ni Benjamin William Mkapa ambaye ndoa yake na Anne Mkapa iliyokuwa na mushkeli kwa muda mrefu, ilipoimarishwa mwaka 1995 baada ya mume kuteuliwa na CCM kuwa mgombea urais.

Baada ya ushawishi wa marafiki kushindikana, viongozi wengine wakiwamo wastaafu walimshauri na kumuomba Anne kupiga moyo konde ili kuimarisha familia na kujenga heshima zaidi ya Mkapa atakapokuwa kiongozi wa juu wa Tanzania. Anne alikubali.

Hali ya ndoa ya Mkapa kabla ya kuwania urais wa Tanzania ndiyo ipo kwa Dk. Hussein Mwinyi aliyepitishwa na chama chake, CCM kuwa mgombea urais wa Zanzibar 2020. Vikao vya juu vya chama hicho vilimpitisha Dk. Mwinyi Julai 10, jijini Dodoma. 

Uchunguzi uliofanywa na timu yetu umebaini kuwa Dkt. Mwinyi na mkewe, Mariam Herman, ambaye wamepata watoto wanne, ndoa yao imekuwa na changamoto kwa muda mrefu, hata kusababisha Agosti, 2018 kutengana.

Hatua hiyo ya kutengana ilisababisha Dk. Mwinyi kuhama nyumba waliyokuwa wakiishi na familia na kwenda eneo jingine. Nyumba hiyo iko eneo la Kawe, Dar es Salaam, mkabala na ofisi za Taasisi ya Benjamin Mkapa.

Sababu kubwa ya kutetereka kwa ndoa ya Dkt. Mwinyi inaelezwa kuwa ni uamuzi wake wa kuwa na mke wa pili. Hatua hiyo haikumfurahisha Mariam ambaye kiasili ni Mkrito. Dkt. Mwinyi ambaye ni mtoto wa Rais (mstaafu) Ali Hassan Mwinyi, ni muislam. Uislam unaruhusu ndoa ya wake hadi wanne.