Vyuma vyakaza zaidi Mwananchi: Waandishi watakiwa aidha kuacha kazi au kubaki kuwa correspondents tu

Kampuni ya Mwananchi Communications Limited, wachapaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti, imewataka waandishi wake wengi kuacha kazi au kubaki kuwa wachangiaji (correspondents).

Wachangiaji katika Vyombo vya Habari hapa nchini hulipwa kwa habari (story) zinazochapishwa, wakati mwandishi hulipwa mshahara kwa mwezi.

Hatua hii inatajwa kuwa ni njia ya kupunguza matumizi kutokana na kukumbwa na mdororo wa uchumi na fedha.

Baada ya kufunga baadhi ya Ofisi za mikoa na kanda na kurejesha waandishi wake makao makuu yake yaliyopo Tabata jijini Dar es Salaam, hatua hii inawaweka waandishi hao njiapanda.

Taarifa tulizozipata zinaeleza kuwa waandishi wengi walipokea barua hizo wameamua kuacha kazi na kuendelea na shughuli nyingine.

“Waandishi wengi, wakiwamo waandamizi, wameamua kuachia ngazi. Hali ni mbaya sana kwa sasa na hatujui hatma yetu,” chanzo kimetueleza.

Mauzo ya gazeti kushuka, COVID-19 vyadaiwa kuchangia

Sababu nyingine tulizoelezwa kuwa zimechangia mdororo huo ni kushuka kwa idadi ya wanunuzi wa magazeti hayo, kukosa matangazo na kupanda kwa gharama za uchapaji na usafirishaji. Pia inaelezwa kushuka kwa wanunuzi wa magazeti hayo kumechangiwa pia na kupungua kwa mzunguko wa fedha kunakochangiwa na mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19.

Usomaji wa magazeti umepeshuka?

Gazeti la Mwananchi hivi sasa linachapishwa nakala zisizozidi 15,000 kwa siku na mabaki yakiwa kati ya asilimia  18-32, huku Mwanaspoti lililokuwa likichapishwa nakala zaidi ya 100,000 sasa linachapa chini ya 50,000 na mabaki asilimia 15. The Citizen lililokuwa likichapishwa nakala 6,000 sasa linachapishwa 4,000 kwa siku huku mabaki yakifikia hadi asilimia 40.