Uchaguzi 2020: Pesa zaanza kuchotwa katika Akaunti ya Akiba ya Fedha za Kigeni

Mchakato wa Uchaguzi Mkuu 2020 wa kupata rais, wabunge na madiwani, utalazimika kutumia kiasi cha fedha kutoka Akiba ya Fedha za Kigeni (GOR).

​Hatua hii inatokana na Serikali kukwama kupata fedha za kutosha kugharamia uchaguzi huo kutoka kwa nchi wahisani kama ilivyozoeleka kwa miaka mingi.

Sehemu kubwa ya fedha za Uchaguzi husimamiwa na Tume ya Uchaguzi Tanzania (NEC) na kwa muda mrefu zilikuwa zikitoka kwa wadau wa maendeleo, hasa UNDP ingawa zinaambatana na masharti kadhaa likiwemo la kuruhusu waangalizi wa kimataifa.

Kwa muda mrefu sasa, Tanzania imekuwa ikilalamikiwa kuwa kinara wa kuminya ustawi wa Demokrasia na kuminywa kwa Uhuru wa Vyombo vya Habari kwa sasa. Vyanzo vyetu vinaeleza kuwa Rais Magufuli alikataa wadau wa maendeleo kutoa pesa za Uchaguzi kwani zilikuwa na masharti ambayo aliona hayatekelezeki na hivyo kwa mara ya kwanza, mwaka 2020 Tanzania itakuwa na Uchaguzi usiokuwa na waangalizi wa kimataifa.

Hifadhi ya fedha za kigeni yaanza kupungua kwa kasi

​Taarifa tulizokuwa nazo hadi jana usiku zinaeleza kuwa kiasi kinachochotwa kwenye akiba hiyo ni Dola za Kimarekani milioni 97.01.

Vyanzo vyetu inaonyesha kuwa Uchaguzi wa mwaka huu unatarajiwa kutumia zaidi ya Shilingi bilioni 300.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Tanzania kulazimika kuingia kwenye akiba hiyo na kuchota fedha ili kuhakikisha Uchaguzi unafanyika.

​Hadi sasa, takwimu kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinasema hadi kufikia mwisho wa mwezi Mei, 2020 akiba ya fedha za kigeni ilikuwa dola za kimarekani Bilioni 5.59.

​Kiasi hicho cha fedha, kwa maelezo ya wachumi, kinaweza kutumika kwa miezi mitano “kuendesha nchi” bila kutegemea mapato ya makusanyo ya kodi na fedha kutoka kwa mataifa rafiki.

Magufuli ameridhia uchotwaji wa fedha hizo

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa tayari Rais Magufuli ameridhia kuchotwa kwa fedha hizo na kuingizwa kwenye mchakato wa Uchaguzi.

Sheria ya matumizi ya akiba ya fedha za kigeni inaeleza kwamba mwangalizi wa fedha hizo ni Rais wa Tanzania, huku BoT ikiwa msimamizi, hivyo matumizi yake lazima yaidhinishwe na ais mwenyewe. 

​Hadi anaondoka madarakani, Rais Jakaya Kikwete, BoT ilikuwa na akiba ya fedha za kigeni dola bilioni 4.4, hivyo katika kipindi cha miaka mitano, Rais Magufuli ameongeza makusanyo ya fedha hizo na kufikisha dola bilioni 5.59 hadi mapema Julai, 2020 ikiwa ni ongezeko la dola bilioni 1.15.