Mbio za kuwania urais wa Tanzania kwa Tundu Lissu, huenda zikafikia ukingoni siku chache baada ya kukabidhi fomu zake Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Lissu alipitishwa na chama chake, CHADEMA kugombea nafasi hiyo katika Uchaguzi wa mwaka huu, 2020 uliopangwa kufanyika Oktoba 28.
Taarifa za uchunguzi zilizopatikana zinaeleza kuwa CCM, Serikali (kwa kutumia Idara ya Usalama wa Taifa) na baadhi ya viongozi wa NEC, wamekuwa wakikutana mara kadhaa jijini Dodoma kupanga mbinu za kuzuia mbio za Lissu.
Miongoni mwa mbinu zinazopangwa ni kuwatumia baadhi ya wagombea wa urais kutoka vyama vya upinzani ili kumuwekea mapingamizi Lissu kwa madai mbalimbali.
Wanaotarajiwa kutumika kuweka mapingamizi ni mgombea urais kupitia chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba na John Shibuda, anayegombea kupitia chama cha ADA-TADEA.
Taarifa zinaeleza kwamba wote wawili wameshazungumzia na wanaopanga mbinu hizo ili kuweka mapingamizi. Shibuda, alizungumza na kigogo mmoja wa Idara ya Usalama, Dar es Salaam siku ya Ijumaa iliyopita.
Shibuda na Lipumba wameandaliwa kuweka mapingamizi makubwa mawili, moja ni kuanza kampeni mapema na jingine ni Lissu kukiuka maadili, kwa madai ya kukiuka maadili kwa kile kilichowekwa kwamba ni “kutukana mgombea – mteule mwenzake.”
Haijafahamika wanaoandaliwa wanalipwa na nani au wameahidiwa nini na nani.
Hata hivyo, uchunguzi wetu umebaini kwamba wagombea hao wawili wanasaidiwa na Serikali kugharimia safari zao na majukumu mengine ya kusaka wadhamini katika mikoa 10. Pia kampeni zao zitasaidiwa na Serikali (mfumo).
Tayari CHADEMA na mgombea wake, Lissu wameeleza kujua kuwepo kwa mpango huo dhidi yao na wanajipanga kuweka wazi (kushitaki) kwa umma.
Leave a Reply