Vyanzo vyetu vya uhakika vinadokeza kuwa huduma ya Mawasiliano ya Mitandao ya kijamii zitaanza kurejea kuanzia kesho Novemba 7.
Mojawapo ya vyanzo vyetu kimetudokeza kuwa watoa huduma (ISP) wameshaanza kupewa maelekezo kuanzia leo warejeshe huduma hiyo ili wananchi wapate kuwasiliana bila vikwazo kama ilivyokuwa hadi tunaandika taarifa hii.
Mitandao mingi ya kijamii ilizuiliwa (blocked) kuanzia Oktoba 27, 2020 ikiwa ni siku moja kabla ya siku ya Uchaguzi Mkuu kitendo kilichopelekea watu wengi kukosa mawasiliano ya kimtandao na wengine kupata hasara kwa kununua vifurushi (bundle) wakidhani vimeisha mapema. Hali hii ilipelekea wananchi kuhamasishana juu ya matumizi ya kiungo mbadala cha siri (VPN) huku wengine wakishindwa kuzipakua baada ya Appstore na Playstore pia kuzuiliwa.
Mitandao iliyozuiliwa ni pamoja na WhatsApp, Twitter, Telegram, Instagram, JamiiForums, YouTube na hata mtandao wetu (imevuja.com).
Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kuchukua hatua hii ambayo wengi wameichukulia kwa hisia tofauti. Hatua hii inaibua mjadala mpya juu ya hatma ya watumiaji wa mitandao na haki yao ya kuwasiliana bila kuingiliwa ambayo ipo kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 18 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2005.
Leave a Reply