Mbowe na Lema walihamishiwa Mlandizi

Viongozi wa CHADEMA, Freeman A. Mbowe, ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Taifa na aliyekuwa Mbunge na mgombea ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless J. Lema walihamishiwa kituo cha Mlandizi mkoani Pwani juzi.

Haijafahamika mara moja lengo la kuwatenganisha na wenzao na sababu hasa za kupelekwa Pwani ingawa chanzo chetu ndani ya Jeshi la Polisi kinabainisha kuwa lengo lilikuwa ni kuepusha ‘msongamano’ wa wanaoenda kuwaona.

Chanzo chetu kimetuhakikishia kuwa hata hao wawili pia hawajui wenzao watakuwa kituo gani kwani mkakati ulikuwa ni kuwatenga na kuwapeleka vituo mbalimbali wakati mashtaka dhidi yao yakiandaliwa.

Afande Mambosasa akiongea na vyombo vya habari alisikika akisema kuwa viongozi hao wa upinzani watafunguliwa mashtaka ya ugaidi kutokana na kuandaa maandamano ya amani kupinga mchakato wa Uchaguzi Mkuu 2020.