TAKUKURU yazidi kung’ata! Ngeleja awekwa ‘mtu kati’. Kigogo wa zamani NDC naye ndani

Baadhi ya wakubwa wa serikali zilizopita, wakiwamo mawaziri, manaibu wao, wakurugenzi wa mashirika, wameanza kuhojiwa na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) kuhusu mkataba wa kuuza hisa za mgodi wa chuma na makaa ya mawe, Liganga na Mchuchuma.

Miongoni mwa vigogo hao ni William Ngeleja, aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, wakati mkataba huo unafungwa kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Sichuan kutoka China.

Mwingine anayeendelea kubanwa kwa mahojiano na TAKUKURU, ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Gideon Nasari. Shirika hilo ndiyo msimamizi wa haki na thamani ya mgodi huo kwa niaba ya Serikali.

Taarifa zilizotufikia zinaeleza kwamba mkataba wa mauziano ya hisa za migodi hiyo iliyoko Mkoa wa Njombe, una harufu ya rushwa.

Hisa kubwa katika mkataba huo inashikiliwa na kampuni hiyo ya China. Wachina waliingia mkataba huo kwa kulipa dola za Marekani bilioni 3 mnamo Septemba, 2011.

Ni kutokana na mazingira hayo, mradi huo mkubwa haujaanza kuzalisha chochote hadi sasa. Rais Magufuli alitoa amri ya kufuatiliwa namna mkataba huo ulivyoingiwa.

Bado TAKUKURU inakusanya ushahidi kwa vigogo hao kabla ya kuchukuliwa kwa hatua nyingine stahiki, zikiwemo za kisheria.