Mwanyika abomolewa akaunti NSSF, alipa TZS Bilioni moja

Michango ya NSSF ya Deogratius Mwanyika, aliyekuwa Rais wa migodi ya Pangea, North Mara Exploration na Bulyanhulu, imelazimika kutumika kulipa sehemu ya fidia ya makubaliano maalum kwa Serikali baada ya kukiri kufanya makosa ya uhujumu uchumi.

Fedha kiasi cha TSh bilioni 1, kilichotwa na kuingizwa kwenye akaunti ya maalum ya fedha za serikali inayosimamiwa na Hazina iliyoko Benki Kuu ya Tanzania (BoT) mnamo Mei 11, 2020.

Makubaliano ya faini yaleta utata hadi Ikulu kuhusishwa

Makubaliano hayo yaliyokuwa na mvutano kiasi hasa katika kuafikiana kiasi cha fedha, Mwanyika akiomba kulipa Sh milioni 700 na serikali kupitia kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), ikisita kuridhia kiasi hicho hadi ilipohusishwa Ikulu mnamo Mei 4, 2020 na kuamua kilipwe kiasi cha TSh bilioni 1.5. Kiasi kingine imekubaliwa kilipwe ndani ya miezi sita.

Juni 17, 2020 Mwanyika aliachiwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, pamoja na wenzake wawili, baada ya Serikali kueleza kwamba Mwanyika amekubali kulipa fidia ya TSh bilioni 1.5. Mwanyika na wenzake wawili, Assa Mwaipopo, mkurugenzi wa migodi hiyo na Alex Lugendo, akiwa Meneja Uhusiano walikutwa na kosa la kukwepa kodi na kuamriwa na Mahakama kulipa faini ya Sh milioni 1.5 kila mmoja.

Kukamatwa na kukiri makosa

Mwanyika na wenzake walikamatwa Oktoba 17, mwaka 2018 na waliendelea kusota rumande gerezani Segerea jijini Dar es Salaam kwa zaidi ya miezi 21 hadi walipoamua kukiri makosa yao; kubwa likiwa ni kuhujumu uchumi. Washtakiwa awali walikuwa na mashtaka 39, lakini 38  yaliondolewa na kubaki moja; kukwepa kulipa kodi, ambalo lilipelekea kupata nafasi ya kulipa faini.

Mshahara wake

Uchunguzi umebaini kuwa Mwanyika aliyefanya kazi katika kampuni hiyo kubwa ya uchimbaji madini, hasa dhahabu kwa zaidi ya miaka 17 – akianzia Kahama Mining kabla ya kuamua kustaafu akiwa na cheo cha Rais wake kanda ya Afrika alikuwa na mshahara wa dola za Marekani 47,300 (sawa na Sh milioni 114) kwa mwezi.

Endapo Mwanyika alidumu katika nafasi hiyo kwa miezi 48 (miaka 4), atakuwa alikusanya zaidi ya Sh 1,104,000,000 (Sh bilioni 1.104). Sheria ya makato ya NSSF kwa wakati huo ilikuwa ikimlazimu mwanachama kulipa asilimia 10 ya mshahara wake huku mwajiri akitakiwa kulipa asilimia kama hiyo na kuingizwa kwenye michango ya mwanachama. Kiasi hiki kwa nafasi hiyo ni tofauti na kile alichohudumu na kuchangia NSSF kwa miaka 13 mingine akiwa na wawekezaji hao.

Mwanyika na michezo yake hatari na wawekezaji

Mwanyika katikati ya wawekezaji hao, alisifika “kupunguza munkari na machungu” kwa wananchi wanaozunguka mgodi wa North Mara baada ya kutokea mauaji ya watu watano na tuhuma za ubakaji zilizokuwa zikielekezwa kwa walinzi pamoja na baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi waliopewa jukumu la kulinda mali za mgodi huo ulioko mkoani Mara.

Katika barua yake ya Machi 11, 2014 ikiwa na kurasa 12, kwa timu ya uchunguzi wa matukio hayo, Umoja wa Mataifa (UN) na wadau wengine wa madini duniani, Mwanyika aliandika barua ndefu kuelezea kilichotokea, hatua zilizochukuliwa na mgodi pamoja na Serikali ya Tanzania na kuahidi kukomesha mauaji na unyanyasaji mwingine dhidi ya binadamu kwa wananchi wanaozunguka na kufanya kazi maeneo ya migodi.

Baada ya hapo, Mwanyika akapewa majukumu makubwa aliyoendelea nayo hadi alipoomba kustaafu mapema kabla ya muda wake.

Ukwasi

Akiwa ni mtaalamu mbobezi wa sheria za madini, Mwanyika amewekeza zaidi kwenye biashara ya hoteli, akiwa na hoteli ya kisasa Njombe, kilimo cha miti na “real estate” jijini Dar es Salaam na Johannesburg nchini Afrika Kusini.