Waandishi wa Habari na Watumishi wa Vyombo vya Habari nchini waliojitokeza kuchukua fomu za kuwania ubunge wamegeuka ombaomba.
Waandishi na watumishi hao wanaofikia 31; huku 29 wakiomba kuteuliwa na chama tawala, CCM na wawili kupitia CHADEMA, wamekuwa wakihaha kusaka fedha ili kufanikisha azma zao.
Uchunguzi wetu umebaini kuwa waandishi waliothibitika kuhangaika zaidi kuomba msaada wa kifedha ni wale waliotia nia kupitia CCM kwa kuwa ndiko wanatakiwa kulipa zaidi wanaporejesha fomu hizo.
Fomu zilikuwa ghali tofauti na matarajio
Ndani ya CCM fomu ya kuwania ubunge ilikuwa ikiuzwa kwa Sh. 100,000 huku kila mgombea akitakiwa kuchangia Sh. 500,000 kukuwezesha chama katika mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa 2020. Ndani ya CHADEMA fomu ilikuwa inauzwa Sh. 100,000 na hakuna michango mingine ya ziada.
Taarifa zinaeleza kuwa pamoja na kwamba CCM hueleza umma kwamba kiasi cha ziada cha Sh. 500,000 ni hiari, lakini wagombea hao wametuthibitishia kwamba ilikuwa lazima na kwamba isipotolewa, mgombea “hana chake.”
Bakuli latembezwa
Katika kuhakikisha waandishi hao wanapata fedha hizo, walianzisha makundi ya WhatsApp ya marafiki, jamaa na ndugu zao ili kukusanya fedha za kufanikisha nia zao.
Taarifa zinaeleza kuwa baadhi ya waandishi wamekuwa wakiwasumbua hata watoa habari wao (sources) ili wasaidie kuwapa michango.
Hatua hiyo inadhihirisha kuwepo kwa hali mbaya ya uchumi kwa vyombo vingi vya habari.
Vyombo vingi vya Habari, magazeti yameshindwa kuwalipa waandishi wao hata mishahara na wengi wanadai hadi stahiki zao za miezi zaidi ya minne.
Hali mbaya ya Vyombo vya Habari inaelezwa kuwa ni kutokana na uchumi wa mtu mmoja mmoja kuwa mbaya baada ya biashara nyingi kufungwa, hivyo ajira za wateja kukoma. Pia inaelezwa kwamba kuminywa kwa uhuru wa Vyombo vya Habari kukosoa serikali na kutishwa kumechangia kudorora mwa mauzo ya magazeti na kukoma kwa matangazo.
Leave a Reply