Pamoja na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais John Magufuli na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally kuonya viongozi wa chama ambao ni wasimamizi kutokuwa na wagombea wao mifukoni, hali imekuwa tofauti majimbo matatu ya mkoa wa Kilimanjaro.
Haya ndo tuliyobaini kwa ufupi na uongozi wa CCM Taifa unaweza kutumia vyanzo vyake kubaini undani wa uchunguzi wetu:
Jimbo la Vunjo
Katika hotuba yake mbele ya mkutano Mkuu wa Jimbo la Vunjo wa kupiga kura ya maoni kuchagua Mbunge, Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Moshi Vijijini, Bwana Cyril Mushi alionekana wazi akimpigia kampeni aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa CRDB, Dkt. Charles Kimei.
Bwana Mushi aliwataka wajumbe kumchagua mgombea ‘mwenye uwezo wa kifedha na mali’ akidai itakuwa rahisi kwa mtu wa aina hiyo kuleta maendeleo kitu ambacho ni kinyume kabisa na Kanuni ya Uteuzi wa Viongozi toleo la Juni 2019.
Pamoja na jitihada za Mushi na genge lake kumkingia kifua Kimei, wajumbe walimkataa na tulipoongea nao walitufahamisha kuwa mtu huyu hana ushirikiano mzuri wa wananchi, hapokei simu na hata kabla ya kura ni mtu aliyekuwa na majivuno y wazi kwao kwani wanadai hata kwenye gari lake hashuki wala kushusha vioo.
Mkakati wa Mushi na Katibu wake, Bi Miriam Kaaya kumbeba Kimei uliambatana na mbinu dhaifu ya kudhibiti vyombo vya habari kushuhudia chochote siku ya mkutano. Waandishi hawakushuhudia hata wagombea wakijinadi na hata wajumbe na wagombea walitakiwa kuzima simu.
Jimbo la Moshi Vijijini
Huku nako Bwana Cyril Mushi na Katibu wake Bi Miriam Kaaya walifanya mchezo mchafu wa kumfanyia kampeni za waziwazi Profesa Patrick Ndakidemi. Bibi Miriam alienda mbali na kutafuta baadhi ya makatibu kata wa CCM Jimbo la Moshi Vijijini na kuwapa maelekezo ya kuhakikisha Profesa anarudi kwa udi na uvumba. Baadhi ya makatibu walituvujishia siri hii. Kulikuwa na fungu ambalo Katibu ndiye aliyelishika na kulisambaza kwa wajumbe.
Jimbo la Moshi Mjini
Aliyeongoza katika matokeo ya kura za maoni Ibrahim Shayo ni ‘mtu wa viongozi’. Huyu alikuwa Meneja wa Kampeni ya Mwenyekiti wa Mkoa wa CCM Bwana Patrick Boisafi wakati alipogombea kura za maoni 2015 akashindwa na wakati akigombea Uenyekiti wa Mkoa mwaka 2017.
Mara baada Boisafi kushindwa kura za maoni na Davis Mosha, Ibrahim Shayo na kundi lao walikisusia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Huyu na genge lake pia walikuwa mtandao wa Membe kwani waliaminishwa na RC wa wakati huo, Leonidas Gama (marehemu) kuwa Rais angekuwa Bernard Membe.
Ibrahim Shayo ambaye ameongoza kura za maoni 2020 Ubunge Moshi Mjini ndiye mwaka 2015 yeye na kundi lake walihakikisha wana CCM hawajitokezi kumdhamini Rais Magufuli alipofika kutafuta wadhamini Kilimanjaro. Aliyeokoa jahazi wakati huo ni aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Profesa Faustine Bee ambaye alitafuta wanafunzi makada wa CCM ndio wakamdhamini.
Kibaya zaidi, mwaka 2015 baada ya Patrick Boisafi kushindwa kura za maoni, yeye na kundi lake la wafanyabiashara wakiongozwa na Ibrahim Shayo wakiwa na hasira pia ya kushindwa kwa Membe, walijiweka pembeni na CCM na wakasaidia upinzani. Kwa sasa ndo mshindi wao wa kura za maoni.
Kabla hata ya kura za maoni, Ibrahim Shayo alifanya kampeni chafu na za waziwazi kwa miaka minne na hakuwahi kuitwa wala kukemewa na viongozi.
Kiuhalisia, Shayo ameongoza kura za maoni kwa kufanya kampeni kwa miaka minne na kubebwa na Mwenyekiti na hata Mwenyekiti jana Julai 24, 2020 amesikika akisema ataenda kumtetea Ibrahim Shayo kwenye NEC ya CCM ili jina lirudi.
Makosa haya yaliwahi kufanywa na CCM mwaka 2010 ambapo mwanachama aliyekuwa abakubalika ni Buni Ramole, lakini Mwenyekiti wa wakati huo, mama Vick Nsilo Swai alipewa fungu la Sh10 milioni na akafunga safari kwenda NEC kutetea jina la Justine Salakana lirudi. Matokeo yake Jimbo likaenda upinzani. Shayo hana ushawishi mbele za wananchi, ni wazi watalipoteza tena jimbo.
Leave a Reply