Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, amewakutanisha maaskofu 71 wa makanisa ya “kiroho” jijini Dar es Salaam akiomba msaada wao ili ashinde ubunge.
Maaskofu hao walikutana Alhamisi iliyopita katika hoteli ya Picolo, iliyoko Kawe jijini Dar es Salaam.
Taarifa zinaeleza kuwa lengo la mkutano huo lilikuwa kuomba viongozi hao wa kiimani kupitia makanisa yao kusaidia Gwajima apate kura nyingi katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu ili awe mbunge.
Kikao hicho kilichoanza saa 5.12 asubuhi, kilianza kwa sala na baadaye wasaidizi wa Gwajima waliendelea na ratiba. Gwajima alifika hotelini hapo saa 4.49 na kwenda moja wa moja kwenye mkutano huo ambao awali ulidaiwa kuwa ulikuwa ni mkutano wa kuombea ‘Amani na Uchaguzi 2020’.
Akishuka katika gari lenye rangi ya kijani aina ya Toyota Prado ambalo lilikuwa limefunikwa namba za usajili kwa bendera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), alisalimia waliompokea na kupelekwa ukumbini.
Baada ya mkutano huo, viongozi hao wa kiroho walipewa bahasha za khaki, ambazo zilionekana kubeba fedha. Haikujulikana haraka ni pesa kiasi gani na sababu za kutolewa kwake.
Leave a Reply