Dk. Bashiru: Wana CCM vumilieni, pesa za kujikimu katika Kampeni zinakuja

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, jana amewaeleza baadhi ya viongozi waandamizi na makada wa chama hicho kuwa wastahimilivu na waache kulalamika kuhusu fedha za kujikimu wakati wa kampeni.

Kumekuwepo na manung’uniko kwa makada wa chama hicho ambao wanazunguka maeneo mbalimbali kuomba kura kwa wagombea wa CCM, kuanzia Rais, Wabunge na Madiwani.

Dk. Bashiru anaelezwa kusema hayo baada ya kusikia malalamiko hayo kutoka kwa makada wanaoambatana na wajumbe wa Kamati Kuu kusaka ushindi katika uchaguzi mkuu unaofanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Taarifa zinaeleza kuwa wengi wanalia njaa, huku wakidai fedha nyingi inapelekwa kwa wasanii lukuki wanaoambatana na wagombea wa chama hicho tawala kwenye kampeni.

Inaelezwa kuwa makada hao wameahidiwa kupewa fedha zao na stahiki zingine kuanzia kesho.

Bashiru aliwahakikishia kuwa fedha zipo na kwamba kila anayefanya kazi atapata stahiki yake.

CCM imepanga kutumia Sh bilioni 17 katika uchaguzi huu, huku ikielezwa kuwa chama hicho kimejipanga kutumia rasilimali ilizonazo kujihakikishia ushindi.