Majasusi wa kimataifa watua nchini, ICC yatuma ujumbe pia

Vitengo vya Usalama katika baadhi nchi na taasisi za kimataifa, vimetuma watu wao kufuatilia kwa karibu mchakato mzima wa kampeni za Uchaguzi wa Tanzania.

Vyanzo vyetu vinaeleza kuwa maofisa wa nchi na taasisi hizo tayari wako nchini wakichunguza mienendo ya viongozi wa vyama, hasa wagombea urais, wakati wa kampeni.

Imebainika kuwa miongoni mwa maofisa hao ni mawakili kutoka Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), yenye makao yake The Hague, Uholanzi; shirika la Human Right Watch (HRW) – New York, Marekani na UN Watch kutoka Geneva, Uswisi.

Mbali na mashirika hayo, pia mataifa makubwa matano yanatajwa kuanzisha madawati maalum katika Balozi zao hapa nchini kufuatilia mchakato huo wa uchaguzi, unaofanyika kila baada ya miaka mitano.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa maofisa hao, baadhi wameingia Tanzania kwa Visa za watalii au kuwa na kazi maalum katika miradi inayosimamiwa na mataifa yao.

Inaelezwa pia kwamba taasisi hizo zimewapa kandarasi ya kuchukua taarifa baadhi ya waandishi wa habari na baadhi ya mashirika yasiyokuwa ya Serikali kwa kazi hiyo.