Nani kawaficha Said Lugumi, Angela Kizigha?

WATANZANIA wawili waliokwapua kifisadi zaidi ya Shilingi bilioni 74, fedha za wananchi, bado wanaonekana mitaani na kwamba “hawagusiki.”

Taarifa za kiuchunguzi zinaeleza kuwa watu hao licha ya kuhojiwa na Vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa zaidi ya mara tano (kila mmoja) hawawezi kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kuwa walifanya ufisadi huo kwa kushirikiana na baadhi ya vigogo waliokuwa ndani ya serikali iliyopita.

Uchunguzi wetu umebaini kuwa watu hao wawili, Said Lugumi ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Lugumi Enterprises na Angela Kizigha, mmiliki wa Daissy General Trade zote za jijini Dar es Salaam wameelekezwa na baadhi ya viongozi wa taasisi za uchunguzi na usalama, “kujificha” na kutopiga kelele kwa muda.

Chanzo chetu kimedokeza “Angela na Lugumi ni kweli wamehojiwa mara kadhaa lakini kuna maelekezo kutoka juu, yaliyotutaka kuchukua taarifa zao na kupeleka majalada yao huko,” .

Uchunguzi wetu umebaini kwamba Angela aliagizwa kutoonekana wala kujichanganya kwenye makundi ya watu na kuepuka kunaswa na vyombo vya habari, masharti ambayo pia alipewa Lugumi.

Tulipofuatilia kutaka kujua kama anayewalinda watu hawa ni Rais Magufuli, chanzo chetu kilidokeza kuwa; “Mimi sijui lakini elewa wametakiwa kutoonekana kwenye kadamnasi mpaka hali itakapopoa.”

Lugumi ajichimbia kijijini, Angela yupo Dar

Imebainika, kwa sasa Lugumi ameweka makazi yake wilayani Magu, Mwanza, wakati Angela amejifungia nyumbani kwake Kijitonyama, Dar es Salaam.

Watanzania hawa wawili tu katika kipindi cha miaka miaka minne, 2014-15 na 2011-12 walikwapua (kwa manufaa binafsi na washirika wao na baadhi ya wakubwa serikalini), kisi hicho kikubwa cha fedha kwa njia ya udanganyifu wa kuhudumia zabuni katika Jeshi la Polisi.

Pesa walizokwapua zingelisaidiaje Taifa?

Kiasi cha fedha kilichokwapuliwa na wawili hawa – takribani 74,000,000,000 (TSh. bilioni 74) endapo kingetumika leo wa ajili ya maendeleo kingeweza kununua magari ya wagonjwa 1,121 na kusambazwa kila hospitali za rufaa, za mikoa na wilaya na mengine yangebaki kwa ajili ya zahanati na vituo vya afya. Tanzania ina jumla ya hospitali 320; zikiwamo za serikali, binafsi na taasisi za dini na mashirika. Gari moja la wagonjwa la kisasa aina ya YinHe kutoka China au Ford Galaxy huuzwa kwa takribani TSh. milioni 66.

Fedha hizo, endapo zingeingizwa katika mfumo na mzunguko rasmi wa serikali, zingeweza kuhudumia bajeti ya Wizara mbili na kiasi kingebaki kwa ajili ya shughuli nyingine za maendeleo na kupambana na umasikini wa Watanzania.

Katika bajeti ya Serikali ya 2020/21, iliyosomwa Bungeni Dodoma mwezi huu, Wizara ya  Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, imepanga kutumia Sh. bilioni 40.2, huku Wizara ya Muungano na Mazingira ikipanga  kutumia Sh. bilioni 27.9, fedha hizi zikijumulishwa, zinafikia kiasi cha Sh. bilioni  68.1. Fedha hizi ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo na mengineyo, ikiwa ni pamoja na mishahara ya wafanyakazi wanaofikia 234 wa wizara hizo kwa mwaka mzima.

Fedha hizo pia zingeweza kujenga barabara ya kilometa 8, na kuhudumia idadi kubwa ya watu, lakini ziliishia kufaidisha familia chache zisizozidi sita, zikiwamo za maofisa kutoka Hazina, Wizara ya Mambo ya Ndani, Jeshi la Polisi na Idara moja nyingine nyeti.

Pesa ilivyopigwa

Kampuni ya Lugumi Enterprises, ilijipatia kwa njia ya udanganyifu TSh bilioni 37 ili kufunga vifaa vya kutambua alama za vidole katika Wilaya 108 nchini, lakini kampuni hiyo ilifunga vifaa katika wilaya 12 na kubainika kuwa kati ya hizo, ni Wilaya nane tu ndiyo zilikuwa zikitumia mfumo huo.

Kampuni ya Daissy General Traders ilipewa zabuni za Sh bilioni 40 na kulipwa kiasi chote. Ilitakiwa kusambaza kofia, sare na makoti ya mvua kwa Jeshi la Polisi, lakini vifaa hivi havikuwahi kuwafikia Polisi hadi sasa.

Wamejineemesha

Kuna haja ya Serikali kufuatilia kwa karibu Mali za hawa watu. Uchunguzi wetu umebaini kuwa Angela ana nyumba zaidi ya 11 Bunju na Mbweni, anazo 2 Kijitonyama, Masaki 1 jijini Dar.

Aidha, Lugumi naye alinunua nyumba jirani na ubalozi wa Marekani uliolipuliwa. Pia ana nyumba Mbweni, Kijichi, n.k huku chanzo chetu kikidai nyumba zake ni ‘mahekalu’.